Tuesday, January 15, 2013

SAFARI YETU MLIMA ULUGURU

Hakika lilikuwa si wazo jepesi kukubalika kwa watu pindi na mara tu nilipotangaza safari ya kuupanda mlima Urugulu hapa mkoani Morogoro kupitia akaunti yangu ya facebook www.facebook.com/edwinshilla, majibu na muitikio haukuwa na mvuto hata. Bali ilionekana kama vile sitopata watu lakini wapi wachache walijitokeza ingawa bado hawakwenda nasi. 

..........Hello! Edwin safari itaaanza saa ngapi?... ndivyo maswali yalivyonijia na nilijibu kama ilivyonipasa. Mwisho wa siku zikatolewa exchuzi na hawakutokea ingawa wenye moyo wa kujitole tulilianzisha asubuhi na mapema siku ya tarehe Desemba 8, 2012. Mimi pamoja na wenzangu King Niver, Meck Touch na Lenny B. tulipanda mlima huo kupitia njia ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kuvuka vijiji mbalimbali na mashamba yenye mazao ya kila aina. Kwa bahati mbaya niling'atwa na Mbwa lakini haikuwa sababu ya kukata tamaa tulisonga mbele na kuvuka camp huko mlimani hasa ile maarufu sana ya Morning Site. 

Kutoka usawa wa bahari mpaka Morning Site Camp ni mwendo wa masaa matatu na nusu,ambapo mtatakiwa kutembea tena kwa mwendo usiopungua masaa manne kufika juu kwenye kilele cha mlima maarufu kwa jina Bondwa. Kwa ujumla mpaka kufika juu ni takribani masaa saba. Ilikuwa ni hali ya kujitolea kwa kweli maana kadili unavyozidi kwenda juu ndivyo ugumu unazidi maana kuna mabonde na miinuko mikali sana huku ikiambatana na chemi chemi za maji pamoja ni miito mnayohitajika kukatisha na kuvuka upande mwingine. 


kwa ugumu huo tulifanikiwa kufika huko juu majira ya saa nane kasoro tangu tulipotoka chini kabisa ilikuwa saa kumi na mbili na nusu asubuhi na mapema. Ukiwa kule juu kabisa huwezi kuuona mji wa morogoro maana ni halisi unakuwa ndani ya wingu jeupe zito lenye baridi kali na mvua za kila mara. Njaa ilituzonga kwa bahati mabaya hatukubeba chakula hata tukiamini maneno ya watu kuwa huko juu wanapika msosi na mtu unatakiwa kununua tu kitu kilichofanya tubebe soda na biskuti tu.

Uzuri tulikutana na walinzi wa mnara wa posta wenye aina mbali mbali za antena za radio na televisheni maarufu hapa nchini tanzania, walitusaidia kwa kutuuzia chakula kwa gharama ya Tsh 1000/= kila mmoja kwa hiyo tulilazimika kulipa Tsh. 4000/= kwa kupikiwa chakula maalufu Tanzania (Ugali, maharagwe na majani ya kunde). 

Tulishiba na kuaanza kujionea maajabu ya uumbaji wa Mungu katika mlima huo. Ndege wazuri, miti mirefu, ukungu mwingi. Ni wazi hakuna kitisho chochote kwenye mlima huo ikiwepo wanyama wakali kama simba, chui, fisi n.k. Zaidi sana utasikia milio ya Ngedere tu ambao hakika hawana madhara yeyote kwa mwanadamu. Hali ya hewa ni nzuri ya ubaridi ambao si kero katika miili yetu iliyozoea joto. 

Baada ya kushangaa yote hayo tulianza safari ya kushuka mlima kurudi mjini majira ya saa kumi na moja jioni amabapo tulifika majumbani mwetu majira ya saa mbili kamili za usiku. Nawasihi ndugu zangu kujiwekea utaratibu wa kuwa na utalii wa ndani na si kuwaachia watu toka nchi za nje kuja kufaidi vya kwetu. Kumbuka "rasilimali za Tanzania ni mali ya kila Mtanzania. Ni vyema kuzitunza kwa kizazi cha sasa na baadae. " Jivunie chako ili kukipa thamani kwa wengine.


 Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Morogoro na kila aishiye humo kwa kutuwezesha kichumi na maendeleo ya kijamii. Amina.

No comments:

Post a Comment

Tafadhali, hakikisha heshima inalindwa kwa kila mmoja wetu. Ni vyema kutii sheria bila shuruti. Ahsante.